Thursday, 7 June 2007

SHERIA YA MIRATHI YA TANZANIA

SHERIA YA USIMAMIZI WA MIRATHI SURA YA 352 YA SHERIA ZA TANZANIA

1. SHERIA HII INASHUGHULIKA NA MAMBO YAPI NA INA LENGO GANI HASA?

Lengo kuu la sheria hii ni kutoa utaratibu wa kusimamia mali za marehemu baada ya kifo chake ikiwamo kuhamisha umiliki wa mali hizo kutoka kwa marehemu kwenda kwa watu wenye haki ya kuzipata mali hizo.Nia hasa ni kwamba mali alizoacha marehemu zisibaki zikiharibika na kupotea bure,au warithi halali au watu wenye maslahi na mali za marehemu,kwa mfano wale wanaomdai hawapotezi haki hiyo, bali awepo mtu ambaye atazisimamia na kuzigawa kwa wahusika wakiwamo wadai na kuepusha mgongano katika jamii husika.Hivyo sheria inamuweka msimamizi wa kugawa mirathi husika na mamlaka yake.

2. MAHAKAMA ZIPI ZINA MAMLAKA YA KUSIKILIZA MASUALA HAYA
Mirathi inaweza kufunguliwa katika mahakama mbalimbali kutegemea na sheria itakayosimamia mirathi husika.

v Kama sheria ya kimila itatumika katika kugawa mirathi basi shauri la kuomba usimamizi wa mirathi litafunguliwa katika Mahakama ya Mwanzo.Msimamizi wa mirathi anatakiwa airidhishe mahakama kwamba marehemu kutokana na maneno yake,mfumo wake wa maisha au maandishi aliyoacha,alionyesha nia kwamba mirathi yake alitaka iendeshwe kwa kufuata sheria za kimila.

v Kama sheria itakayotumika ni ya kiisilamu basi shauri la kuomba usimamizi wa mirathi litafunguliwa Mahakama ya Mwanzo.Msimamizi wa mirathi anatakiwa airidhishe mahakama kwamba marehemu kutokana na maneno yake,mfumo wake wa maisha au maandishi aliyoacha,alionyesha nia kwamba mirathi yake alitaka iendeshwe kwa kufuata sheria za kiislamu.


v Kama sheria itakayotumika kugawa mirathi ni ya Serikali basi mahakama wilaya,mahakama ya hakimu mkazi na mahakama kuu zinahusika kutegemea thamani ya mali alizoacha marehemu.

· Thamani ya mali yote aliyoiacha marehemu isiyoondosheka isiyozidi shilingi milioni 5 (Mfano nyumba, mashamba) na inayoondosheka isiyozidi shilingi milioni 3 (mfano magari) mirathi ya aina hii inafunguliwa Mahakama ya Mwanzo.
· Thamani ya mali yote aliyoiacha marehemu isiyohamishika isiyozidi shilingi milioni 12 na inayohamishika isiyozidi shilingi milioni 100 mirathi hii inafunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ama ya Hakimu Mkazi.
· Thamani ya mali inayozidi shs millioni 150 mirathi hii inafunguliwa mahakama Kuu.

3. SHERIA IMETAJA WATU WA AINA GANI AMBAO WANAWEZA KUWA WASIMAMIZI WA MIRATHI?

A] Ndugu wa marehemu na wale wenye maslahi na mirathi ya marehemu,kwa mfano wale ambao wanatarajia kupata sehemu ya mirathi ya marehemu.

B] Mtu au watu wanaomdai marehemu,Mtu huyu hufungua mirathi pale ambapo ndugu wa marehemu wameshindwa au hawataki kufungua mirathi.

C] Kkabidhi wasii mkuu, huyu au hii ni ofisi ya serikali ambayo hujihusisha,Pamoja na mambo mengine,usimamizi wa mirathi,endapo itaombwa na mtu yeyote.

D] Muwakilishi wa kisheria mtu aliyetajwa kama msimamizi wa mirathi [mtu aliyepewa power of attorney]

E]Mtu yeyote ambaye mahakama kwa kuangalia vigezo mbalimbali vikiwamo udugu,maslahi ya muhusika katika mirathi hiyo,usalama wa mali za mirathi pamoja na uwezekano wa kuisimamia vizuri,anaweza kuteuliwa na mahakama

VILEVILE Sheria imetoa baadhi ya vigezo ambavyo mtu lazima awe navyo ali apate usimamizi wa mirathi
I]awe mtu mzima
Ii]awe na akili timamu


4. KUNA NAMNA NGAPI ZA UTOAJI WA MAMLAKA YA USIMAMIZI WA MIRATHI
Namna ya kutoa usimamizi wa mirathi hutegemea jinsi marehemu alivyojiandaa kukutana na kifo chake,kuna wengine huacha wosia na wengine huwa hawaachi wosia.
A] KAMA KUNA WOSIA
Kama kuna wosia usimamizi wa mirathi hupewa mtu yule tu aliyetajwa kwenye wosia,mtu huyo anaweza kuwa ametajwa moja kwa moja au kwa hali halisi ilivyojionyesha kwenye wosia kwamba lazima atakuwa ni yeye.Hivyo kuandika wosia ni nafasi pekee ya kuchagua msimamizi wa mirathi.

Vile vile mtoa wosia anaweza kuchagua mtu zaidi ya mmoja kusimamia mirathi yake.Ikumbukwe kuwa kuna wosia za aina mbili.Ya kwanza ni wosia wa maandishi na wa pili ni ule wa maneno.Wosia wa maneno ni lazima uthibitishwe kwa ushahidi wa wahusika ambao ulitolewa mbele yao.Pale ambapo mahakama itajiridhisha na uwepo wa wosia na ikatoa amri ya usimamizi itakuwa imethibitisha usahihi wosia husika.Wosia wa maandishi nao lazima uthibitishwe angalau kwa kuleta mtu aliyeshuhudia ukiandikwa ili athibitishe kwamba marehemu alikuwa na akili timamu wakati akiandika wosia huo na hakulazimishwa na mtu yeyote.

B] WOSIA ULIOMBATANISHWA NA BARUA YA USIMAMIZI WA MIRATHI
Hii hutokea katika mazingira yafuatayo

i] Pale ambapo marehemu ameacha wosia lakini wosia huo haujamtaja mtu ambaye amarehemu alitaka awe msimamizi wa mirathi yake

ii] Pale ambapo watu wote waliotajwa na marehemu katika wosia kwamba wasimamie mirathi yake wamekataa hoja hiyo au ni watu ambao kisheria hawana uwezo wa kusimamia mirathi,kwa mfano mtoto,mtu asiye na akili timamu

iii] Pale ambapo wasimamizi wote wa mirathi walitajwa katika wosia wamefariki kabla mwandika wosia hajafariki au amefariki kabla ya kumaliza kazi yake ya usimamizi wa mirathi.
Katika hali kama hii,lazima ndugu wakae wachague mtu ambaye wamempendekeza kuwa msimamizi wa mirathi na watatakiwa waende mahakamani na wosia huo ili wakaombe mahakama imthibitishe rasmi.Hapa ndipo amri ya usimamizi wa mirathi ukiwa na wosia ulioambatanishwa na barua ya usimamizi wa mirathi hutolewa.



C] KAMA HAKUNA WOSIA
Kama marehemu hakuacha wosia wowote,barua za usimamizi wa mirathi zinaweza kutolewa kwa mtu yoyote ambaye kwa mujibu wa taratibu za usimamizi wa mirathi zinazohusika katika mirathi hiyo[za kimila au za kiserikali au za kiislamu] atakuwa ana haki ya kupata mali zote za marehemu au sehemu ya mali hizo.Pale inapotokea mtu zaidi ya mmoja ameomba usimamizi wa mirathi ya marehemu,mahakama itakuwa na utashi wa kuchagua mmoja au mtu zaidi ya mmoja kusimamia mali za marehemu,na katika kufanya hivyo mahakama inatakiwa kisheria iangalie mtu mwenye maslahi makubwa zaidi naya karibu na mirathi hiyo kuliko yule mwenye maslahi madogo.Vile vile kama itatokea kwamba marehemu alikuwa anadaiwa,na hakuna ndugu aliyefungua mirathi ya marehemu mahakamani,basi mdai ana uwezo wa kuomba kufungua mirathi husika
Mahakama inapoona kwamba ni muhimu au ni busara kumchagua mtu ambaye katika hali ya kawaida asingechaguliwa kusimamia mirathi,mahakama,kwa kuangalia ukaribu wa kiundugu,maslahi aliyonayo muhusika katika mirathi,usalama wa mirathi husika na uwezekano wa mirathi hiyo kusimamiwa vyema,itamchagua mtu huyo asimamie mirathi.






D] USIMAMIZI WA MIRATHI KWA MAMBO MAALUMU.
I] USIMAMIZI WA MIRATHI WAKATI SHAURI LIKIENDELEA KUSIKILIZWA
Inawezekana kwamba
-bado kuna ubishi mahakamani kuhusu uhalali wa wosia,au
shauri la kuomba kupata barua ya usimamizi wa mirathi kwa mtu ambaye hakuacha wosia bado linaendelea au
-shauri la kuomba mahakama izifute barua za usimamizi wa mirathi alizopewa mtu Fulani linaendelea ,
-mahakama ina uwezo wa kuteua msimamizi wa muda wa mali za marehemu huku kesi ikiendelea mahakamani.Msimamizi huyu atakuwa na mamlaka kamili kama aliyo nayo msimamizi ma kudumu wa mali za marehemu isipokuwa tu haruhusiwi kugawanya mali za marehemu.Vilevile msimamizi huyu atakuwa chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa mahakama. Ili muhusika apate ruksa hii ni lazima atoe sababu za kuonesha dharura ya ombi husika na umuhimu wakeSuala hili limekuwa likiwatatiza hasa hasa akina mama na watoto.Inaweza kutokea watoto bado wanasoma shule na baba yao akafariki.Baba ana mali nyingi pengine ana akaunti benki.Lakini pengine ndugu au watu wowote bado wanabishana mahakamani kwamba ni nani ana haki ya kusimamia mirathi.Ni mara nyingi inatokea mahakama inaruhusu akina mama hawa kuchukua kiasi Fulani cha pesa kulipa ada za watoto wao,kuwatibu,hata matumizi ya muhimu ya nyumbani bora tu wasijihusishe na kugawa mali za marehemu.


ii] MTEULIWA WA KUSIMAMIA MIRATHI BADO ANA UMRI MDOGO

Pale ambapo mtu anayatakiwa kusimamia mirathi bado ana umri mdogo,usimamizi wa muda hupewa mtu mzima ambaye atakuwa ameteuliwa na mahakama kama mwangalizi wa mtoto na mali zake au kwa mtu yeyote ambaye mahakama itaona anafaa mpaka pale muhusika atakapokuwa mtu mzima na kuwa na uwezo wa kusimamia mali zake vizuri.

Iii] MTEULIWA WA KUSIMAMIA MIRATHI HANA AKILI TIMAMU
Pale ambapo mtu anayetarajiwa kusimamia mirathi hana akili timamu,mahakama itamteua mtu ambaye atasimamia mirathi hiyo kwa muda na kwa faida ya muhusika mpaka pale atakapokuwa na uwezowa kiakili wa kuisimamia mirathi husika

Iii] USIMAMIZI WA MIRATHI KWA AJILI YA KUKUSANYA NA KUTUNZA MALI ZA MAREHEMU
Kama inaonekana ni muhimu kwamba mali za marehemu zikusanywe na kuhifadhiwa pahal pamoja,mahakama inaweza kutoa usimamizi huo kwa mtu yoyote ambaye anafaa ili afanye kazi hiyo ikiwa ni pamoja na kulipa madeni lakini haruhusiwi kugawa mali kwa warithi

5. UTARATIBU UTUMIKAO KATIKA KUOMBA USIMAMIZI WA MIRATHI MAHAKAMANI
A. KAMA KUNA WOSIA WA MAREHEMU

1. Taarifa ya kifo iandikishwe kwa mkuu wa wilaya ndani ya siku 30

2. Msimamizi wa mirathi aende akafungue mirathi mahakamani akiwa na
a]wosia uliachwa na marehemu
b]Cheti cha kuthibitisha kifo cha marehemu
3. Mahakama hutoa tangazo la maombi ya kuteuliwa msimamizi wa mirathi kwa muda wa siku 90, lengo la tangazo ni kwamba kama mtu yeyote ana pingamizi dhidi ya wosia au msimamizi wa mirathi basi awasilishe mahakamani.Kama hakuna tatizo lolote msimamizi hukabidhiwa barua ya kuhalalisha uteuzi wake na majukumu yake

B.KAMA HAKUNA WOSIA WA MAREHEMU
1. Kifo kiandikishwe kwa mkuu wa wilaya ndani ya siku 30

2. Mkutano wa ukoo ufanyike kuchagua msimamizi wa mirathi

3. Msimamizi wa mirathi aende kufungua mirathi mahakamani akiwa na nakala ya uamuzi wa ukoo na cheti cha kifo

4. Tangazo hutlewa na mahakama kwa muda wa siku 90.Kama hakuna matatizo,msimamizi hukabidhiwa barua ya kuhalalisha usimamizi wake





6. SHERIA IMEWAPA WAJIBU UPI WASIMAMIZI WA MIRATHI?
Kazi ya usimamizi wa mirathi ni kazi ambayo inahitaji uaminifu wa hali ya juu,na ningependa wasikilizaji wa Redio one wawe makini katika kuchagua watu hawa kutokana na madaraka makubwa ambayo sheria inawapa.Uchaguzi mbaya wa msimamizi wa mirathi umeleta madhara makubwa kwenye familia nyingi na mali nyingi imepotea.Hebu tuangalie mamlaka ya msimamizi wa mirathi.

1.Huyu atakuwa ndio muwakilishi halali wa kisheria wa mambo yote ya marehemu na mali zote za marehemu kisheria zitakuwa chini yake kama msimamizi na sio kwamba ni mali yake,katika kesi ya
-MOHAMED HASSAN Vs MAYASA MZEE AND MWANAHAWA MZEE [1994] T.LR 225 mahakama ya rufaa iliamua kwamba kisheria msimamizi wa mirathi halazimiki kupata ruhusa ya warithi kabla ya kuuza mali yoyote ya marehemu.

-Katika kesi ya AZIZ DAUDI AZIZ Vs AMIN AHMED ALLY&ANOTHER CIV. App No30 of 1990[unreported] mahakama ya rufaa iliamua kwamba pale tu msimamizi wa mirathi anapoteuliwa,mali zote zinakuwa chini ya mamlaka yake kama msimamizi na anachukua majukumu ambayo alikuwa nayo marehemu kwenye mali yake wakati yu hai.Msimamizi huyu huachiwa kuamua jinsi ya kushughulikia mirathi hiyo kadri atakavyoona inafaa


2. Atakuwa na mamlaka ya kufungua mashitaka mahakamani kwa niaba ya marehemu au kushitakiwa kwa niaba ya marehemu na atawajibika kulipa madeni ya marehemu kutoka katika mali alizoacha marehemu.

3.Msimamizi wa mirathi vilevile atakuwa na uwezo wa kuhamisha umiliki wa mali za marehemu kama atakavyoona inafaa kwa kuziweka rehani,kuziuza au kuzikodisha,kwa kuzingatia maslahi ya warithi na watu wanaomdai marehemu.Hivyo msimamizi wa mirathi hawezi tu kuamka na kutangaza kuuza mali za marehemu bila sababu za msingi.

4. Atawajibika kutumia kiasi Fulani cha pesa za marehemu kwa ajili ya kutunza mali za marehemu ziwe katika hali nzuri na zisiharibike.

5. Msimamizi wa mirathi anatakiwa ndani ya miezi sita tangu apewe usimamizi au ndani ya muda mahakama ambao itaona unafaa, anatakiwa apaleke mahakamani na kuonyesha mali zote za marehemu na thamani yake halisi, madeni yake anayodaiwa au anayodai marehemu na ndani ya mwaka mmoja msimamizi wa mirathi atatakiwa tena kama mahakama itakavoona inafaa, aonyeshe mali za marehemu zilizo mikononi mwake na jinsi alivyozifanya au kuzishughulikia.

Mahakama ina uwezo wa kuendelea kumuongezea muda muhusika kadri itakavyoona inafaa. Lakini kama msimamizi wa mirathi atatakiwa na mahakama kuonyesha mali za marehemu na akashindwa kufanya hivyo ndani ya muda aliopewa,atakuwa ametenda kosa la jinai na akipatikana na hatia atatakiwa lipe faini ya shillingi elfu mbili au apewe kifungo cha miezi sita.

Na kama ataonyesha mali hizo kwa nia ya kudanganya au kuficha atakuwa ametenda kosa la jinai ambalo kifungo chake ni miaka saba.Mtu yeyote mwenye maslahi na mirathi anao uwezo wa kufanya ukaguzi ili kujiridhisha na usimamizi wa mirathi ya marehemu

6.Msimamizi wa mirathi vile vile anatakiwa akusanye mali za marehemu na madeni aliyokuwa akidai na kulipa madenialiyokuwa akidaiwa,Katika madeni aliyokuwa anadai marehemu ni vizuri msimamizi wa mirathi akayadai mapema ili yasije yakapitwa na wakati kisheria

6. Msimamizi wa mirathi hatakiwi kujipatia faida kutokana na usimamizi wa mirathi hiyo,na kama msimamizi wa mirathi yeye mwenyewe au kwa kupitia kwa mtu mwingine atanunua mali ya marehemu,uuzaji huo unaweza kukataliwa kisheria na mtu yeyote mwenye maslahi na mirathi hiyo .Moja ya sababu ya kufanya hivyo ni kwamba kuna uwezekano mkubwa akajiuzia mali hizo kwa bei ya chini kuliko thamani halisi ya mali husika.

7. Vile vile ni jukumu la msimamizi wa mirathi kutoa fedha kwa ajili ya shughuli za mazishi ya marehemu,ila gharama hizo ziangalie hali halisi ya maisha ya marehemu na kama ameacha kiasi cha mali cha kutosha kwa ajili ya shughuli hiyo.Kama msimamizi wa mirathi alitoa fedha yake kwa ajili hiyo na haki ya kwanza ya kulipwa fedha zake kabla ya madni mengine ya marehemu.



7.JE WATU WANAOTARAJIA KUFAIDIKA NA MIRATHI WANA HAKI ZIPI ZA KISHERIA KUFUATILIA USIMAMIZI WA MIRATHI

I] HAKI YA KUMTAKA MSIMAMIZI ASIMAMIE MIRATHI AU AJIONDOE
Haki hii anayo mtu yeyote mwenye maslahi na mirathi ya marehemu,ambapo anaweza kumtaka aje mahakamani na kufanya zoezi la usimamizi wa mirathi au ajiondoe katika usimamizi kama aliteuliwa kwa wosia au na ukoo. Hii mara nyingi hutokea pale ambapo msimamizi wa mirathi bila sababu za msingi anachelewesha kufungua mirathi na mali za marehemu zinaendelea kupotea bure.Muhusika asipotokea mahakamani itachukuliwa kwamba amekataa uteuzi uliofanywa katika wosia wa usimamizi wa mirathi.Ni vizuri kuchukua hatua hii mapema lakini kwa umakini kwa kuwa katika kipindi hiki inaweza kutokea msimamizi huyu akaenda mahakamani kimya kimya akapata uthibitisho wa mahakama na akachezea mali za marehemu na warithi wakabaki wanateseka




ii] HAKI YA KUWEKA PINGAMIZI
Mtu yeyote ambaye anaona ana haki au ana maslahi na mirathi ya marehemu anaweza kuweka pingamizi mahakamani dhidi ya mtu ambaye anaomba kupewa usimamizi wa mirathi.Lengo la kuweka pingamizi ni kuiambia mahakama kwamba mtu aliyeomba kupewa usimamizi wa mirathi asipewe haki hiyo mpaka mtu aliyetoa pingamizi apewe taarifa.
Pingamizi hili linaweza kuwa na sababu mbalimbali ikiwamo kuangalia kama wosia una uhalali, uaminifu wa muhusika na tabia yake kwa ujumla.Haitarajiwi familia ikubali mtu mwenye historia ya jinai apewe usimamizi.Pingamizi hili litakuwa na nguvu ya kisheria kwa muda wa miezi mine na baada ya hapo lazima liwekwe pingamizi jingine ili kulipa uhai lile la kwanza.Baada ya hapo mahakama husikiliza pingamizi hilo.

iii]HAKI YA KUKAGUA MAENDELEO YA KAZI YA USIMAMIZI WA MIRATHI
Mtu yeyote anayetarajia kufaidika na mali za marehemu kutokana na wosia au hata kama hakuna wosia au mtu yeyote anayemdai marehemu ana haki ya kukagua listi ya mali iliyopelekwa mahakamani na msimamizi wa mirathi.Hii husaidia kuepusha udanganyifu unaofanywa na wasimamizi wengi wa mirathi kwa kuficha baadhi ya mali za marehemu.




iv] MGAO WAKE HALALI


8. JE NI SABABU ZIPI ZINAZOWEZA KUSABABISHA MAHAKAMA IKAMUONDOA MSIMAMIZI WA MIRATHI?
Mahakama inao uwezo wa kufuta haki ya usimamizi wa mirathi ikiwa kuna sababu za msingi za kufanya hivyo.Sheria imezitaja sababu hizo katika kifungu cha 49 kama ifuatavyo.

A] Kama mwenendo mzima wa kupata haki ya usimamizi wa mirathi ulikuwa na kasoro kubwa. Hivyo kuathiri kabisa usahihi wa kesi husika.Kwa mfano shauri hilo limefunguliwa kwenye mahakama ambayo haina mamlaka ya kusikiliza suala husika, kama muhusika amefariki mwanza halafu shauri likafunguliwa dare s salaam,au utolewaji wa mirathi ulifanywa bila kujumuisha watu ambao ilikuwa ni lazima wajumuishwe

B] kama mtu amepewa haki ya kusimamia mirathi kwa maoni yasiyo sahihi,kwa mfano pale ambapo wahusika wameghushi wosia au wametumia wosia ambao marehemu aliufuta wakati wa uhai wake




C] vile vile kama muhusika amepata usimamizi wa mirathi kwa kuelezea mambo yasiyo ya kweli,kwa mfano kusema uongo kuhusu mahali marehemu alikuwa akiishi au mahali mali zake zilipo,au pale ambapo mwanamke anasema yeye alikuwa ni mke wa marehemu wakati si kweli

D]pale ambapo usimamizi wa mirathi umeonekana hauna maana tena au haufanyi kazi.Kwa mfano
-pale ambapo Juma amepata usimamizi wa mirathi ikiaminika kwamba marehemu hakuacha wosia halafu wosia halisi umepatikana au
-pale mtu aliyepewa usimamizi wa mirathi amekuwa hana akilitimamu,
-au pale ambapo usimamizi wa mirathi umekamilika huwezi tena kufuta usimamizi hata kama wosia utapatikana

E] Pale ambapo msimamiziwa mirathi kwa makusudi ameshindwa kuleta listi ya mali za marehemu na jinsi alivyozishughulikia

Sababu ambazo haziwezi kufanya usimamizi wa mirathi ufutwe nipamoja na
I] kutoelewana kwa kawaida kati ya wasimamizi wa mirathi
Ii] Kuacha kuleta listi ya mali za marehemu bila kukusudia




9. MSIMAMIZI WA MIRATHI AKIITUMIA VIBAYA MIRATHI HIYO AU AKIWA MZEMBE KATIKA KUSIMAMIA MIRATHI,MAHAKAMA INAWEZA KUMWAJIBISHA ALIPIE HASARA ALIYOSABABISHA?
Msimamizi wa mirathi ni kama mdhamini wa mali za marehemu na anawajibika kwa kuwa mdhamini.

A] KUSIMAMIA VIBAYA MIRATHI
Endapo msimamizi wa mirathi atasimamia mirathi vibaya anawajibika binafsi kwa matokeo ya usimamizi huo mbaya.Kwa mfano
-msimamizi wa mirathi analipa madai ambayo hakutakiwa kulipa,au
-anachanganya pesa za mirathi na zake binafsi,au
-anawekeza pesa za mirathi katika biashara zake mwenyewe,hapa kisheria inahesabika kwamba amejikopesha na anatakiwa adaiwe riba awe amepata faida au la.
-Mfano mwingine ni pale msimamizi wa mirathi anapouza mali za marehemu kwa thamani ya chini kuliko thamani halisi.

B] KUSABABISHA HASARA AU UHARIBIFU KATIKA MALI ZA MIRATHI
Mfano mmoja wa hasara ni pale ambapo marehemu alikuwa anadaiwa na benki kiasi Fulani cha pesa,msimamizi wa mirathi,japokuwa ana pesa za kutosha,halipi deni hilo,riba anaendelea kupanda kila siku mpaka inafikia mamilioni,hapa msimamizi wa mirathi amesababisha hasara na inabidi yeye ndiye awajibike


C] KUWAJIBIKA KWA UZEMBE
Kushindwa kwa msimamizi wa mirathi kuzikusanya mali za marehemu au
-kuziuza mali za marehemu ambazo labda najua zitaharibika mapema na kuweka pesa benki
- pale ambapo msimamizi wa mirathi anajua kabisa kwamba marehemu alikuwa anamdai mtu Fulani,lakini msimamizi wa mirathi hafuatilii hilo deni mpaka linapitwa na wakati kisheria,hapa msimammizi wa mirathi inabidi awajibike kulipa kiasi hicho cha pesa alichoshindwa kukidai.



SHERIA ZINAZOTOA UTARATIBU WA JINSI YA KUGAWA MIRATHI YA MAREHEMU NCHINI TANZANIA

1. KUNA SHERIA NGAPI AMBAZO HUTUMIKA KUGAWA MIRATHI YA MAREHEMU NCHINI TANZANIA.

Tanzania kuna sheria nne ambazo hutumika katika kugawa mirathi ya marehemu.

SHERIA YA INDIA YA MIRATHI YA MWAKA 1865
Sheria ya kwanza ni Sheria ya India ya Mirathi ya Mwaka 1865,ambayo inatumika Tanzania kwa mujibu wa Sheria namba 2 inayoruhusu matumizi ya baadhi ya sheria za India nchini Tanzania.Mojawapo ya sheria hizo ni sheria hii ya Mirathi.Itakumbukwa kwamba Tanzania pamoja na India zilitawaliwa na Mkoloni mmoja ambaye ni muingereza,hivyo alichokuwa akifanya mkoloni huyu ni kuamuru kwamba sheria Fulani inayotumika India basi itumike na Tanganyika.

SHERIA ZA MIRATHI YA KIMILA
Jamii ya Tanzania ina makabila mengi,na kila kabila lina mila zake.Mila ni desturi zilizoshamiri au zilizotumika kwa muda mrefu na kukubalika katika jamii hizo na zikipata nguvu ya kisheria huitwa sheria za kimila.Sheria hii hutumika kwa watanzania wote wazawa wasio na asili ya kizungu,kiasiaau kisomali.

SHERIA YA MIRATHI YA KIISLAMU
Watanzania wote ambao itadhihirika kuwa wameacha mila na desturi zao na ambao Uislamu huwaongoza katika vipengele vyao vyote vya maisha yao,pamoja na watu wengine ambao sio wazawa lakini ni waislamu hupaswa kutumia sheria ya kiislamu katika mirathi yao.

SHERIA YA MIRATHI YA WATU WENYE ASILI YA KIASIA WASIO WAKRISTO SURA YA 28 YA SHERIA YA TANZANIA
Sheria hii inaruhusu kutumika kwa sheria za mirathi za dini za watu wenye asili ya kiasia lakini sio wakristo.Hii huwajumuisha wahindu pamoja na dini nyingine zisizo za kikristro zinazopatikana katika bara la asia.


2. MAMBO GANI HUANGALIWA KABLA YA MAHAKAMA KUAMUA KUCHAGUA KUTUMIA AINA MOJAWAPO YA SHERIA HIZO.
Kwa kawaida mfumo wa kugawa mali za marehemu kama hajaacha wosia huwa umepangwa tayari na sheria za nchi,dini au mila.Lakini hata hivyo kuna wakati ambapo hutokea utata wa sheria ipi itumike kwa mtu Fulani hasa pale ambapo marehemu labda alikuwa mtu wa kabila Fulani na wakati huio huo ni muislamu au mkristu.Pale unapotokea mgongano wa aina hiyo kuna mambo mawili ambayo huzingatiwa na mahakama

A] MAISHA ALIYOKUWA AKIISHI MAREHEMU

B] NIA YA MAREHEMU
Kama muhusika atathibitisha kwamba marehemu aliachana kabisa na mila zake,basi sheria nyingine hutumika

3. TUANZE NA SHERIA YA MIRATHI YA KISERIKALI YA INDIA YA MWAKA 1865, SHERIA HII INATUMIKA KWA WATU GANI.

Sheria hii hutumika kwa watanzania wote walioacha mila na desturi zao na ambao sio waislamu pamoja na watu wengine ambao sio wazawa.Mara nyingi huchukuliwa kwamba watu wanaokaa mijini muda mrefu wameacha kufuata misingi yao ya mila ya jamii zao,japo sio lazima sana mtu atakuwa maeacha misingi hiyo ya kimila ya asili yake.

4. SHERIA HII YA MIRATHI YA KISERIKALI IMETOA UTARATIBU GANI WA KUGAWA MALI?

[A]KAMA MUME KAFARIKI AKAACHA MJANE NA WATOTO NA NDUGU WENGINE
Kama mume kafariki akaacha mjane na watot,moja ya tatu ya mali za mumewe zilizo kwenye mirathi anatakiwa apewe mke wake,na mbili ya tatu ya mali hizo itaenda kwa watotot wake.Na kama hakuna watoto katika familia husika,mali hiyo hugawanywa kwa ndugu kupewa nusu mna mjane kupewa nusu ya mirathi ya marehemu..
Na kama marehemu hajaacha ndugu,mali yote huchukuliwa na mjane.

[B]KAMA MJANE AMESHAFARIKI NA MUME HANA NDUGU MWINGINE YEYOTE

[C]KAMA MKE AMEFARIKI NA KAMUACHA MUME,NI NINI HAKI ZA MUME KWENYE MIRATHI YA MKEWE
Mume naye ana haki kama alizo nazo mke ya kupata mirathi kutoka katika mali za marehemu.Hivyo mume hupata moja ya tatu ya mali za marehemu mkewe na mbili ya tatu huenda kwa watoto.Kama hakuna watoto ila kuna ndugu wa mke tu,basi nusu ya mali huenda kwa mume na nusu huenda kwa ndugu wa mke.N kama mke hana ndugu,mume huchukua mali zote za mkewe

D] KAMA AMEBAKI MTOTO TU AU WATOTO TU NA WAZAZI WAMEFARIKI
Sheria inasema kwamba kama wazazi wa watoto wote wamefariki,basi mali za marehemu hupewa mtoto,kama yuko peke yake huchukua zote,kama wapo wengi,basi watoto hao hugawana mali hizo sawa kwa sawa bila kujali ni mwanamke au mwanaume anayepata mali husika

[E]KAMA WAZAZI WAMEFARIKI NA WATOTO WAO WOTE WAMEFARIKI,NA WAMEBAKI WAJUKUU AU MJUKUU MMOJA
Kama wazazi wamefariki na watoto wao nao pia wamefariki lakini wakaacha wajukuu,basi mali hiyo hugawiwa kwa mjukuu huyo au wajukuu hao sawa kwa sawa
[F] KAMA MTOTO KAFARIKI LAKINI BABA YAKE YU HAI
Baba huchukua mali yote ya mirathi
[G]KAMA BABA AMEFARIKI AKAACHA MAMA YAKE MZAZI NA KAKA ZAKE NA DADA ZAKE WAKO HAI
MIRATHI KATIKA SHERIA ZA KIMILA
11. SHERIA INASEMA MILA NINI?

12. SHERIA ZA KIMILA ZIMEGAWANYIKA KATIKA MIKONDO MINGAPI?
Sheria za kimila zimegawanyika katika sehemu mbili

A]MKONDO WA BABA
Sheria za kimila tulizo nazo Tanzania na ambazo zimewekwa katika maandishi na serikali ni sheria za kimila zilizokusanywa toka kwenye makabila yanayorithi kufuata ukoo wa baba.Sheria hizi zimo katika kanuni za Urithi Tangazo la serikali namba 436 la mwaka 1963

B] MKONDO WA MAMA
Hizi ni sheria za kimila ambazo zinayahusu makabila ambayo hurithi kupitia upande au ukoo wa mama.Kwa bahati mbaya sheria hizo za kimila hazijawekwa katika maandishi kama ilivyo katika sheria za urithi kupitia upande wa baba.

13. KIMILA URITHI UMEGAWANYWA KATIKA MADARAJA MANGAPI
Katika sheria kimila Urithi umegawanyika katika makundi matatu

A] DARAJA LA KWANZA
Kwa kawaida ni mtoto wa kwanza wa kiume wa ndoa.Kama mume ana wake wengi basi mtoto wa kwanza wa kiume wa mke mkubwa.Kama mke mkubwa hana mtoto wa kiume basi mtoto wa kiume wa mke mdogo.Huyu hurithi fungu kubwa kuliko wote.


B] DARAJA LA PILI
Daraja hili linajumuisha watoto wote wa kiume waliosalia ambao hurithi sehemu kubwa kuliko watoto wa kike ambao ni daraja la tatu

C]DARAJA LA TATU
Daraja la tatu ni watoto wote wa kike bila kujali umri wao au nafasi yao ya kuzaliwa.Hawa hupata sehemu ndogo kuliko wote.Kama hakuna watoto wa kiume watoto wa kike hupata urithi zaidi.Kanuni hizo zimeweka wazi kwamba watoto wa kike hawaruhusiwi kurithi ardhi ya ukoo ila wanaruhusiwa kuitumia tu mpaka watakapoolewaau kufa.Hawana mamlaka ya kuiuza.Pamoja na kanuni hii,mahakama Kuu ya Tanzania[Mwanza]katika kesi ya Benardo Ephraim dhidi ya HOLARIA PASTORI ilitamka kuwa sheria hiyo inayobagua watoto wa kike kurithi ardhi ya ukoo ni batili


14. JE WATOTO WA NJE YA NDOA WANARITHI?
Mahakama ya Rufaa katika kesi namaba 72 katika ripoti ya sheria ya mwaka 1990 kati ya VIOLET ISHENGOMA dhidi ya KABIDHI WASII MKUU NA MWENZAKE imetoa tafsiri ya mtoto katika sheria ya ndoa kwamba haihusishi mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa hivyo,watoto hao hawatambuliwi chini ya sheria ya ndoa kama watoto.
Watoto walizaliwa nje ya ndoa hawaruhusiwi kurithi,wanaweza kurithi tu kama wamehalalishwa kwa kufuata desturi au taratibu zinazojulikana na kutambulika katika jamii hiyo.
Vilevile inashauriwa kwamba ni muhimu kuandika wosia ambao katika kugawa mali utamjumuisha mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa.Hii itasaidia kuondoamateso yanayowapata watoto walizaliwa nje ya ndoa.

15. KATIKA SHERIA ZA KIMILA MJANE ANA HAKI YA KURITHI?
Mjane hakutajwa katika madaraja ya urithi kwa mujibu wa sheria hii ya kimila.Mjane inabidi aishi kwa kutegemea watoto wake ambao watarithi mali ya baba yao.
-iwapi marehemu hakuacha watoto wala wajukuu kaka na dada zake waliochangia baba na mama ndio warithi.Kaka wa kwanza atakuwa daraja la kwanza ambaye atapata sehemu kubwa,kaka waliobaki watakuwa daraja la pili ambao watapata sehemu kubwa kuliko daraja la tatu ambao ni wanawake
-Ikiwa marehemu hakuacha kaka wala dada,basi mali hiyo hurithiwa na watoto wa kaka na dada zake kama wapo
-Kama wote hawapo,baba wa marehemu anaweza akarithi
-Iwapo baba hayupo,baba wadogo watarithi
-Kama baba wadogo hawapo shangazi atarithi
-Kama shangazi hayupo,ndugu wengine watarithi
Kazi ya warithi siku zote ni kumtunza mjane na kuwagawia sehemu ya mali zinazoondosheka.


MIRATHI KATIKA SHERIA ZA DINI YA KIISLAMU
16. SHERIA YA DINI YA KIISLAM HUTUMIKA KWA WATU GANI HASA
Watanzania wote ambao itadhihirika kuwa wameacha mila na desturi zao na ambao Uislamu huwaongoza katika vipengele vyao vyote vya maisha yao,pamoja na watu wengine ambao sio wazawa lakini ni waislamu hupaswa kutumia sheria ya kiislamu katika mirathi yao.

17. SHERIA YA KIISLAMU INASEMAJE KUHUSU URITHI
Wenye kurithi katika wanawake ni kumi (10) wafuatao:
1. Binti (mtoto mwanamke)
2. Binti wa mtoto mwanamume (mjukuu)
3. Mama
4. Dada wa kwa baba na mama
5. Dada wa kwa baba
6. Dada wa kwa mama
7. Bibi mzaa baba
8. Bibi mzaa mama
9. mke
10. Bibi mwenye kuacha mtumwa huru.
Wenye kurithi kwa wanaume ni kumi na tano (15). Watu hao ni:
1. Mtoto mwanamume
2. Mtoto mwanamume wa mtoto mwanamume (mjukuu)
3. Baba
4. Baba wa kwa baba
5. Ndugu mwanamume wa kwa baba na mama
6. Ndugu mwanamume wa kwa baba tu
7. Ndugu mwanamume wa kwa mama tu.
8. Mtoto mwanamume wa kwa ndugu mwanamume wa kwa baba na mama
9. Mtoto mwanamume wa ndugu mwanamume wa kwa baba tu
10. Ami (baba ndogo) wa kwa baba na mama (ndugu yake baba).
11. Ami wa kwa baba tu
12. Mtoto mwanamume wa Ami wa kwa baba na mama
13. Kijana mwanamume wa ami wa kwa baba
14. Mume
15. Bwana mwenye kumwacha mtumwa huru.
Kuzuiliana
Tumeona kuwa wanaume wenye kurithi ni 15 na wanawake wanaorithi ni 10. Lakini wote hawa 25 wakikutana pamoja hawawezi kuruthi wote bali baadhi yao hawazuuilia wengine wasipate kitu au wasipate fungu kubwa. Katika kipengele hiki tutaonyesha wanazuiliwa na wasio zuiliwa.
1. Mtoto mwanamume hazuiliwi na mtu
2. Mjukuu huzuliwa na mtoto mwanamume na kila mtoto wa kiumbne aliyeko mbali huzuiliwa na aliyoko karibu na marehemu
3. Baba hazuiliwi na mtu
4. Babu wa upande wowote huzuiliwa na baba au babu wa karibu zaidi (k.m. baba yake baba humzuilia babu yake baba).
5. Ndugu wa kwa baba na mama huzuiliwa na mtoto mwanamume au mjukuu au baba.
6. Ndugu wa kwa baba huzuiliwa na ndugu wa kwa baba na mama; na kila amzuiliaye yeye (huyo ndugu wa na mama; na kila amzuiliaye yeye (huyo ndugu wa kwa baba na mama) vile vile huzuiliwa na dada wa kwa baba na mama akiwa pamoja na binti au binti wa mtoto wa kiumbe (mjukuu) au wote wawili.
7. Ndugu wa kwa mama huzuiliwa na mtoto au mtoto wa mtoto mwanamume au baba au babu.
8. Mume hazuiliwi na mtu wala
9. Mke hazuiliwi na mtu
10. Binti hazuiliwi
11. Mama hazuiliwi
12. Bibi huzuiliwa na mama.
Mafungu yenye Kurithiwa.
Mafungu ya uruthi yaliyotajwa katika Qur'an (4:11-12) ni haya sita yafuatayo:
1. Nusu (1/2)
2. Robo (1/4)
3. Thuluthi (1/3)
4. Thuluthi mbili (2/3)
5. Sudusi (1/6)
6. Thumuni (1/8).
Mwenye kupewa mafungu
Katika warithi kuna wenye kupata mafungu maalum katika hayo mafungu sita; na kuna wasiokuwa na mafungu maalum ambao hupata kilichobakia baada ya wenye mafungu kuchukua mafungo yao au hupata mali yote ikiwa hapana wenye mafungu. Wasio na mafungu huitwa ASABA.
Wenye mafungu maalum katika urithi ni watu kumi na mbili (12) wafuatao:
1. Baba
2. Babu
3. Binti
4. Binti wa mtoto mwanamume (mjukuu)
5. Ndugu wa kwa mama
6. Dada wa kwa baba na mama
7. Dada wa kwa baba
8. Dada wa kwa mama
9. Mama
10. Bibi
11. Mume
12. Mke.
Asaba - Warithi wasio na mafungu maalum.
Asaba ni warithi wasio wekewa fungu maalum na kustahiki kupata mali yote ikiwa hapana mwenye fungu au kupata kilicho bakia baada ya wenye mafungu kuchukua haki yao. Asaba wenyewe wako wa aina tatu:
(a) Asaba kwa nafsi yake
(b) Asaba wa pamoja na mtu mwingine
(c) Asaba kwa sababu ya mtu mwingine
(a) Asaba kwa nafsi yake ni wale wanaume tu ambao uhusiano wao na huyu marehemu haukuingiliwa namwanamke. Nao ni hawa wafuatao:
1. Mtoto mwanamume
2. Baba
3. Baba
4. Babu (baba yake baba)
5. Ndugu wa kwa baba na mama
6. Ndugu wa kwa baba
7. Mtoto mwanamume wa ndugu wa kwa baba na mama
8. Mtoto mwanamume wa ndugu wa kwa baba
9. Ami wa kwa baba na mama
10. Ami wa kwa baba
11. Mtoto mwanamume wa Ami wa kwa baba na mama
12. Mtoto mwanamume wa ami wa kwa baba
13. Bwana na bibi mwenye kumuacha mtumwa huru
14. Asaba wa mwenye kuacha huru mtumwa.
(b) Asaba wa pamoja na mtu mwingine ni hawa wafuatao:
1. Binti akiwa pamoja na kijana mwanamume
2. Binti wa mtoto wa kiume (mjukuu) akiwa pamoja na mtoto mwanamume wa mtoto mwanamume (mjukuu wakiume)
3. Dada wa kwa baba na mama akiwa pamoja na ndugu wa kwa baba na mama.
4. Dada wa kwa baba akiwa pamoja na ndugu wa kwa baba
5. Dada wa kwa baba na mama au wa kwa baba akiwa pamoja na babu.
(c) Ama Asaba kwa sababu ya mtu mwingine ni dada wa kwa baba na mama au wa kwa baba tu atakapokuwa pamoja na binti au binti wa mtoto wa kiume au wote wawili.
Musharakah - Kushirikiana Fungu
Ingawa Asaba wote utaratibu wao wa kurithi ni mmoja lakini nani kati yao mwenye haki zaidi ya kurithi pindi wakitokea pamoja itategemea na uzawa wa karibu na uwiano wa uhusiano wa maiti. Kwa mfano, uhusiano wa kwa baba na mama una nguvu zaidi kuliko uhusiano wa kwa baba tu, kwa hiyo, asaba wa kwa baba na mama ana haki ya kurithi kuliko asaba wa kwa baba tu.
Tumefahamu kwamba, asaba hana fungu, bali huchukua urithi wote kama hakuna mwenye fungu, au huchukua kilicho haki baada ya wenye mafungu kuchukua chao au hukosa kabisa kama hakuna kilichobakia au wakati mwingine asaba wenye daraja sawa na mwenye fungu, watashirikiana fungu hilo. Kwa mfano: Amekufa mtu akaacha mume, mama, ndugu wa kwa mama zaidi ya mmoja na ndugu wa kwa baba na mama.
Ugawaji wa Mirathi:
- Mume ana nusu (1/2) = 3/6
- Mama ana sudusi (1/6) = 1/6
- Ndugu wengine wa kwa mama wana thuluthi (1/3) = 2/6.
Hapo utaona kuwa mafungu yote sita yamegawiwa ya kaisha na ndugu wa kwa baba na mama hawakupata kitu. Hapa itabidi ile thuluthi waliyoipata ndugu wa kwa mama wagawane sawa sawa na ndugu wa kwa baba na mama maana nao wanayo haki ya ndugu wa kwa mama kama wao na wala hakoseshwi kwa sababu ya uasaba wake.
Kurithisha kwa kutumia mifano mbali mbali
Wakikutana warithi na pakawa hapana amzuiliaye mwenziwe na ikawa wote ni Asaba, wataigawanya mali iliyopo sawa sawa kwa kadri ya idadi yao. Kwa mfano, akifa mtu, akawa ameaacha vijana wanaume wanne, mali yote itagawanywa mafungu manne sawa sawa na kila mmoja apewe fungu lake.
Ama wakikutana asaba wanaume na wanawake, basi kila mwanamume atahesabiwa kuwa ni wanawake wawili, na mali itapigwa mafungu kila mwanamume mmoja apewe mafungu mawili na kila mwanamke apewe fungu moja. Kwa mfano, amekufa mtu akaacha watoto sita, wanne wanaume na wawili wanawake. Wanaume wanne watahesabiwa kuwa ni sawa na wanawake wanne. Kwa hiyho mali itagawanywa katika mafungu kumi yaliyo sawa sawa. Wanaume watapata mafungu mawili kila mmoja na wanawake watapata fungu moja moja.
Iwapo warithi ni mchanganyiko wa wenye mafungu maalum na asaba, itabidi kutafuta kigawe kidogo cha shirika (lowest common multiple (LCM) ili kupata mafungu yatakayhogawiwa kwa kila mrithi kwa kadri ya haki yake anayoistahiki. Hebu tuangalie mifano kadhaa ya mgawanyo wa mirathi.
Kwa mfano 1:
Amekufa mke na kuacha:
i) mume
ii) mtoto mwanamume
iii) baba
Wenye mafungu maalum kati ya hawa ni:
i) mume - ana robi (1/4) madhali yupo mtoto
ii) baba ana sudusi (1/6) madhali yupo mtoto.
Asaba Mtoto mwanamume na atachukua kitakacho bakia.
Ugawaji
Mafungu yatakayotolewa ni 1.4 na 1.6. Hesabu ndogo ambayo inaweza kutolewa mafungu ya urithi ni 12 yaani LCM ya 4 na 6. Kwa hiyo mali ya uryhtii itagawanywa kwenye mafungu 12 yaliyo sawa sawa na ugawaji utakuwa kama ifuatavyo:
i) Mume atapata 1/4 ya 12 (1/4 x 12) = 3
Yaani atachukua mafungu 3 katika mafungu 12 = (3/12 - 1/4)
ii) Baba atapata 1/3 ya 12 (1/6 x 12) = 2 yaani atachukua mafungu 2 kati ya mafungu 12 - (2/12 = 1/6).
iii) Mtoto atachukua mafungu yaliyobakia 12 - (3 + 2) = 7, yaani atachukua mafungu 7 kati ya mafungu 12 - (7/12)
Mfano wa 2:
Amekufa mume na kuacha wafuatao:
- mke mmoja
- mama
- mjukuu mmoja wa kike (binti wa mtoto mwanamume)
- mtoto mwanamume
- watoto watatu wanawake.
Kama mali iliyoachwa na marehemu ni Shs. 1,200/-, utarthisha wahusika kama ifuatavyo:
Ugawaji:
Wenye mafungu maalum kati ya hawa ni:
- Mke ambaye atapata thumuni (1/8) kwa sababu wapo watoto
- Mama atapata sudusi (1/6) ya mali kwa sababu wapo watoto.
Mjukuu hapati kitu kwa sababu wapo watoto ambao humzuilia
- Mtoto mwanamume na watoto wanawake watagawana mali iliyho bakia, wakiwa hao Asaba mwanamume achukue sawa na wanawake wawili (2:1).
Njia mbili zifuatazo zinaweza kutumika katika kurithisha wahusika:
(a) Hisabu ndogo inayoweza kutolewa mafungu ni 24. Yaani LCM ya 8 na 6. Kila fungu litakuwa na thamani ya Shs. 50 - (1,200 + 24). Kwa hiyo:
- Mke atapata 1/8 ya 24 (1/3 x 24) = 3 yaani atapata 3 x 50 = 150/=.
- Mama atapata 1.6 ya 24 (1/6 x 24) = yaani atapata mafungu 3 ambayo ni sawa na shs. (4 x 50) = 200/=.
- Asaba watarithi mali iliyobakia ambayo ni 1,200 - (150 + 200) = 850/-.
Mali hii itagawanywa katika mafungu 5 (kumbuka: mwanamume atapata sawa na wanawake wawili). Hivyo, kila mtoto wa kike, atapata Shs.1 x 850/- = 170/- na mtoto wa kiume, atapata Shs. 2 x 850 = 340/- .
(b) Njia ya pili ni kutafuta sehemu ya mali atakayoipata kila mwenye fungu maalum. Kama mali inayorithiwa ni Shs. 1,200/-.
- Mke atapata 1/8 ya 1,200/- = 1/8 x 1200 = 150/=
- Mama atapata 1/6 ya 1,200 = 1/6 x 1200 = 200/-.
Asaba watagawana mali iliyobakia ambayo ni 1200 - 350 = 850/-.
Kuna binti 3 na kijana mmoja ambaye ni sawa na binti 2. Hivyo mali iliyo bakia itagawanywa katika mafungu 5 ambapo kila binti atapata = Shs. 1 x 850 = 170/-.
na kila mama watapata sawa na binti 2 Shs. 2 x 850 = 340/-.
Kuongeza Mafungu (Awl) Iwapo idadi ya mafungu yatakayogaiwa kwa warithi wenye mafungu maalum ni kubwa kuliko mafungu yaliyopatikana kwa njia ya LCM, idadi ya mafungu itabidi iongezeke ili kila mmoja apate haki yake.

10 comments:

Anonymous said...

Muda gani ambao mtu mwenye maslahi katika mirathi aende mahakamani kudai haki yake katika mirathi. Mfano: mume wangu amekufa, mirathi imefunguliwa na nimepata taarifa kuwa mirathi imefunguliwa nimekaa kimya miaka 20 ikapita. Je nina haki gani katika kudai haki yangu. Sheria ya ukomo inasemaje kwa mtu kama mimi.

kawau said...

Mimi ni mvulana wa miaka 28 na ni mtoto pekee wa marehemu baba yangu. Alifariki nikiwa na miaka 16 na msimamizi wa mirathi alikuwa mama yangu mzazi. Sasa tatizo linakuwa hivi... mama yangu hajanishirikisha katika lolote mpaka sasa,na baadhi ya mali za marehemu baba yangu anazifuja,ikiwemo kuuza nyumba moja na kiwanja. Katika kumbu kumbu zangu alinishirikisha kitu kimoja tu alipo uza nusu ya kiwanja. Licha ya hizo marehemu baba yangu aliacha
fremu za biashara na nyumba mbili pamoja na kiwanja kimoja. Na hakuna hata kimoja ambacho nimeshirikishwa . Na nimejihudumia mwenyewe na kujisomesha bila msaada wake toka 2005 elimu ya juu mpaka hivi sasa. Je sheria na haki yangu ni ipi?? Napenda kufahamu...

Unknown said...

MIMI NI MATTHEW MARTIN. . . BABA YANGU ALIFARIKI JUNE 4\6/2012. . . . MPAKA SASA SIJUI KINACHOENDELEA SERIKALINI. . . . .NA SIJUI NI MUDA GANI HUCHUKUA KWA MFANYAKAZI KUPATA MIRATHI ENDAPO ITAKUWA HAKUNA MIGOGORO YOYOTE. . MAANA WATOTO NI WANAFUNZI.

wa bruno said...

SISI MAHAKAMA WANATUSUMBUA MPAKA BASI, WANATAKA RUSHWA TU

Unknown said...

Naomba kuuliza

Unknown said...

Kama marehemu kafariki ana watoto wa wili wakike na wakiume njee na kila mtoto na mama yake Ina kuwaje .na mama wamarehemu yupo hai anafaidikaje

Unknown said...

Naomba msaada plz no zangu 0788062771 naomba mwanasheria anisaidie

tavonjagielski said...

TiG Metal: Titanium Mesh, Iron Frame, and Steel Rings
TiG metal-steel-ring infiniti pro rainbow titanium flat iron rings-rings and gold jewelry are titanium jewelry piercing unique and unique to their jewelry. The titanium grades ring, ring, and silver jewelry are titanium phone case designed titanium dioxide formula

Anonymous said...

Habari Yako.
Unakosea sana na isitoshe Inaonyesha elimu uliyosoma haijakusaidia,Mirathi apo inakuhusu asilimia 95 huyo ni mama Yako sawa ila kudai Haki Yako sio kujitenga nae.
Pambana ktk Haki kuleta heshima ya Mali ya baba Yako.Anza kuongea na mama Yako mkumbushe kuwa Mali ni ya baba Yako na muulize haki Yako iko wapi?Akileta ubishi na asikupe majibu ya Amani na ushirikiano basi hiyo sio mama anaeitakia vyema kesho Yako.Hivyo tafuta ofisi ya mkuu wa wilaya anzia kupeleka malalamiko Yako apo utapata msaada.Uenda umepata shida kujisomesha Lakini mama anafuja Mali na mabwana wengine au na watu wengine.

Anonymous said...

Nenda Kwa mkuu wa wilaya